Jumapili. 28 Aprili. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 3 ya Mwaka (Jumatano, Januari 24, 2024)  

Somo la 1

2Sam 7:4-17

Neno la Bwana likamfikia Nathani kusema, Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani. Mahali mwote nilimokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lo lote na mtu ye yote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi? Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, Bwana wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani. Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; naam, kama vilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena Bwana anakuambia ya kwamba Bwana atakujengea nyumba. Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu; lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele. Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi.

Wimbo wa Katikati

Zab 89:3-4, 26-29

Nimefanya agano na mteule wangu,
Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu.
Wazao wako nitawafanya imara milele,
Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele.
(K) Hata milele nitamwekea fadhili zangu.

Yeye ataniita, Wewe baba yangu,
Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza,
Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.
(K) Hata milele nitamwekea fadhili zangu.

Hata milele nitamwekea fadhili zangu,
Na agano langu litafanyika amini kwake.
Wazao wake nao nitawadumisha milele,
Na kiti chake cha enzi kama siku za mbingu.
(K) Hata milele nitamwekea fadhili zangu.

Injili

Mk 4:1-20

Yesu aliaanza kufundisha tena kando ya bahari. Wakamkusanyikia mkutano mkubwa mno, hata yeye akapanda chomboni, akakaa baharini, mkutano wote ulikuwako juu ya nchi kavu kando ya bahari. Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, akawaambia katika mafundisho yake, Sikilizeni; Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda; ikawa alipokuwa akipanda, mbegu nyingine ilianguka kando ya njia, wakaja ndege wakaila. Nyingine ikaanguka penye mwamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara ikaota kwa kuwa na udongo haba; hata jua lilipozuka iliungua, na kwa kuwa haina mizizi ikanyauka. Nyingine ikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea ikaisonga, isizae matunda. Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia. Akasema, Aliye na masikio ya kusikilia, na asikie. Naye alipokuwa peke yake, wale watu waliomzunguka, na wale Thenashara, walimwuliza habari za ile mifano. Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano, ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije wakaongoka, na kusamehewa. Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje? Mpanzi huyo hulipanda neno. Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao. Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha; ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa. Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno, na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai. Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia.

Maoni


Ingia utoe maoni