Masomo ya Misa
Jumanne ya 3 ya Mwaka (Jumanne, Januari 23, 2024)
2Sam 6:12–15, 17-19
Daudi alienda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumb ya Obed-edomu mpaka mji wa Daudi, kwa shangwe. Hata ikawa, watu waliolichukua sanduku la Bwana walipokwisha kwenda hatua sita, akachinja ngómbe na kikono. Daudi akacheza mbele za Bwana kwa nguvu zake zote; na Daudi na nyumba yote ya Israeli wakalileta sanduku la Bwana kwa shangwe, na kwa sauti ya tarumbeta.Wakaliingiza sanduku la Bwana, na kuliweka mahali pake, katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake; naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana. Kisha Daudi alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani akawabarikia watu kwa jina la Bwana wa majeshi. Akawagawia watu wote, makutano wote wa Israeli, wanaume kwa wanawake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate wa zabibu. Basi watu wote wakaenda zao, kila mtu nyumbani kwake.
Zab 24:7-10
Ndiye Bwana, Mfalme wa utukufu.
Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
Inukeni, enyi malango ya milele,
Mfalme mtukufu apate kuingia.
(K) Ni nani mfalme mtukufu?
Ni nani mfalme wa utukufu?
Bwana mwenye nguvu hodari,
Bwana hodari wa vita.
(K) Ni nani mfalme mtukufu?
Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
Naam, viinueni, enyi malango ya milele,
Mfalme wa utukufu apate kuingia.
(K) Ni nani mfalme mtukufu?
Ni nani huyu Mfalme wa utukufu?
Bwana wa majeshi,
Yeye ndiye mfalme wa utukufu.
(K) Ni nani mfalme mtukufu?
Mt 11:25
Aleluya, aleluya,
Utukuzwe Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya.
Mk 3:31-35
Wakaja mamaye na nduguze wa Yesu; wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita. Na makutano walikuwa wameketi, wakimzunguka; wakamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta. Akawajibu, akisema, Mama yangu na ndugu zangu ni akina nani? Akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana mtu yeyote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.
Maoni
Ingia utoe maoni