Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 2 ya Mwaka (Jumamosi, Januari 20, 2024)  

Somo la 1

2Sam 1:1-4, 11-12, 17-19,23-27

Ikawa baada ya kufa kwake Sauli, hapo Daudi aliporudi katika kuwaua Waamaleki, naye Daudi amekaa siku mbili katika Siklagi; hata siku ya tatu ikawa, tazama! Akaja mtu kutoka kambi ya Sauli, nguo zake zimeraruliwa, tena ana mavumbi kichwani mwake; basi, ikawa alipomfikia Daudi, akaanguka chini, akamsujudia. Daudi akamwambia, Umetoka wapi? Akamwambia, Nimeokoka katika kambi ya Israeli. Daudi akamwambia, Yalikwendaje? Tafadhali uniambie. Akajibu, Watu wamekimbia vitani, tena watu wengi wameanguka wamekufa; hata Sauli naye na Yonathani, mwanawe, wamekufa.Ndipo Daudi akashika nguo zake akazirarua na kadhalika watu wote waliokuwa pamoja naye; wakaomboleza, wakalia, wakafunga hata jioni, kwa ajili ya Sauli, na kwa ajili ya Yonathani mwanawe, na kwa ajili ya watu wa Bwana na kwa ajili ya nyumba ya Israeli; kwa sababu wameanguka kwa upanga. Basi Daudi akamwomboleza Sauli, na Yonathani, mwanawe, maombolezo haya; (kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Yashari), akasema, Wana wa Yuda na wafundishwe haya, Walio fahari yako, Ee Israeli Juu ya mahali pako palipoinuka wameuawa; Jinsi mashujaa walivyoanguka! Sauli na Yonathani walipendwa na kupendeza Maishani wala mautini hawakutengwa; Walikuwa wepesi kuliko tai, Walikuwa hodari kuliko simba. Enyi binti za Israeli, mlilieni Huyo Sauli, ambaye aliwavika Mavazi mekundu kwa anasa, Akazipamba nguo zenu dhahabu. Jinsi mashujaa walivyoanguka Katikati ya vita! Ee Yonathani, wewe umeuawa Juu ya mahali pako palipoinuka Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, Ulikuwa ukinipendeza sana; Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, Kupita upendo wa wanawake. Jinsi mashujaa walivyoanguka, Na silaha za vita zilivyoangamia!

Wimbo wa Katikati

Zab 80:1-2, 4-6

Wewe uchungaye Israeli, usikie, 
Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi; 
Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru. 
Mbele ya Efraimu, na Benyamini, na Manase, 
Uziamshe nguvu zako, Uje, utuokoe. 
(K) Ee Mungu, uangazishe uso wako nasi tutaokoka

Ee Bwana, Mungu wa majeshi, hata lini Utayaghadhibikia maombi ya watu wako? 
Umewalisha mkate wa machozi, 
Umewanywesha machozi kwa kipimo kikuu. 
Unatufanya sababu ya ugomvi kwa jirani zetu, 
Na adui zetu wanacheka wao kwa wao. 
(K) Ee Mungu, uangazishe uso wako nasi tutaokoka

Injili

Mk 3:20-21

Yesu aliingia nyumbani na mkutano wakakusanyika tena, hata wao wenyewe wasiweze hata kula mkate. Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili.

Maoni


Ingia utoe maoni