Jumapili. 12 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 2 ya Mwaka (Alhamisi, Januari 18, 2024)  

Somo la 1

1Sam 18:6-9; 19:1-7

Walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile. Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi. Lakini huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi. Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi, nakusihi, ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha; na mimi nitatoka nje na kusimama kando ya babangu huko shambani ulipo wewe, nami nitazungumza na babangu habari zako; nami nikiona neno lo lote nitakuambia. Naye Yonathani akamsifu Daudi kwa Sauli, babaye akamwambia, Mfalme asikose juu ya mtumishi wake, yaani, juu ya Daudi kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako yamekuwa mema sana. Kwa kuwa alitia uhai wake mkononi mwake, na kumpiga yule Mfilisti, naye Bwana akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona jambo hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue huyo Daudi bure? Sauli akaisikiliza sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, Aishivyo Bwana, yeye hatauawa. Basi Yonathani akamwita Daudi, naye Yonathani akamjulisha mambo hayo yote. Kisha Yonathani akamleta Daudi kwa Sauli, naye alikuwa akihudhuria mbele yake, kama kwanza.

Wimbo wa Katikati

Zab 56:1-2, 8-12

Mungu, unirehemu, maana yuko atakaye kunimeza,
Mchana kutwa ananionea akileta vita.
Adui zangu wanataka kunimeza mchana kutwa,
Maana waletao vita juu yangu kwa kiburi ni wengi.
(K) Nimemtumaini Mungu sitaogopa

Umehesabu kutanga-tanga kwangu;
Uyatie machozi yangu katika chupa yako;
(Je! Hayamo katika kitabu chako?)
Ndipo adui zangu watarudi nyuma siku ile niitapo.
(K) Nimemtumaini Mungu sitaogopa

Neno hili najua kuwa MUNGU yu upande wangu;
Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake.
Kwa msaada wa Bwana nitalisifu neno lake.
(K) Nimemtumaini Mungu sitaogopa

Nimemtumaini Mungu, sitaogopa;
Mwanadamu atanitenda nini?
Ee Mungu, nadhiri zako zi juu yangu;
Nitakutolea dhabihu za kushukuru.
(K) Nimemtumaini Mungu sitaogopa

Injili

Mk 3:7-12

Yesu alijitenga, yeye na wanafunzi wake, akaenda baharini. Mkutano mkuu ukamfuata, kutoka Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu, na Idumaya, na ng'ambo ya Yordani, na pande za Tiro na Sidoni, mkutano mkuu, waliposikia habari za mambo yote aliyokuwa akiyatenda, wakamwendea. Akawaambia wanafunzi wake ya kwamba chombo kidogo kikae karibu naye, kwa sababu ya mkutano, wasije wakamsonga. Maana aliponya wengi, hata wote waliokuwa na misiba wakamrukia wapate kumgusa. Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu. Akawakataza sana, wasimdhihirishe.

Maoni


Ingia utoe maoni