Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 1 ya Mwaka (Jumamosi, Januari 13, 2024)  

Somo la 1

1Sam 9:1-4, 17-19; 10:1

Kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini, jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu. Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, kijana, tena mzuri; wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wote. Na punda za Kishi, baba yake Sauli, walikuwa wamepotea. Kisha akamwambia Sauli mwanawe, Haya basi, twaa mtumishi mmoja pamoja nawe, uondoke, uende ukawatafute punda hao. Naye akapita kati ya nchi ya milima milima ya Efraimu, akapita na kati ya nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona; kisha wakapita kati aya nchi ya Shaalimu, wala huko hawakuwako; wakapita kati ya nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwapata. Hata Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu. Ndipo Sauli akamkaribia Samweli langoni, akasema, Tafadhali uniambie, nyumba ya mwonaji iko wapi? Samweli akamjibu Sauli, akasema, Mimi ndimi mwonaji; tangulia mbele yangu ukwee mpaka mahali pa juu, kwa maana mtakula pamoja nami leo; kisha, asubuhi nitakuacha uende zako, nami nitakuambia yote uliyo nayo moyoni mwako. Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema, Je! Bwana hakukutia mafuta uwe mkuu juu ya watu wake Israeli? Nawe utamiliki watu wa Bwana, na kuwaokoa na mikono ya adui zao; kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa Bwana amekutia mafuta uwe mkuu juu ya urithi wake.

Wimbo wa Katikati

Zab 21:1-6

Ee Bwana, mfalme atazifurahia nguvu zako,
Na wokovu wako ataufanyia shangwe nyingi sana.
Umempa haja ya moyo wake,
Wala hukumzuilia matakwa ya midomo yake.

Maana umesogezea Baraka za heri,
Umemvika taji ya dhahabu safi kichwani pake.
Alikuomba uhai, ukampa,
Mda mrefu wa siku nyingi, milele na milele.

Utukufu wake ni mkuu kwa wokovu wako,
Heshima na adhama waweka juu yake.
Maana umemfanya kuwa Baraka za milele,
Wamfurahisha kwa furaha ya uso wako.

Injili

Mk 2:13-17

Yesu alitoka, akaenda kando ya bahari, mkutano wote ukamwendea, akawafundisha. Hata alipokuwa akipita, akamwona Lawi wa Alfayo, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaondoka akamfuata. Hata alipokuwa ameketi chakulani nyumbani mwake, watoza ushuru wengi wa wenye dahmbi waliketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwamaana walikuwa wengi wakimfuata. Na waandishi na Mafarisayo walipomwona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.

Maoni


Ingia utoe maoni