Masomo ya Misa
Ijumaa ya 1 ya Mwaka (Ijumaa, Januari 12, 2024)
1Sam 8:4-7, 10-22
Wazee wote wa Israeli walikutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama; wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote. Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba Bwana. Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao. Naye Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya Bwana. Akasema, Mfalme atakayewamiliki ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, kwa magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake. Naye atawaweka kwake kuwa maakida juu ya elfu, na maakida juu ya hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake. Na binti zenu atawatwaa kuwa wafanyaji wa marhamu, na wapishi, na waokoaji. Atatwaa Makonde yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake. Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape maakida wake, na watumishi wake. Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng’ombe zenu walio wazuri sana, na punda zenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe. Atawatoza fungu la kumi la makundi yenu; nanyi mtakuwa watumwa wake. Nanyi mtalia siku ile kwa sababu ya mfalme wenu mliyejichangulia; Bwana asiwajibu siku ile. Walakini hao watu wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu; ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu atuamue, tena atoke mbele yetu na kutupigia vita vyetu. Samweli akayasikia maneno yote ya watu, akayanena masikioni mwa Bwana. Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti yao, ukawafanyie mfalme.
Zab 89:15-18
Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe,
Ee Bwana, huenenda katika nuru ya uso wako.
Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa,
Na kwa haki yako hutukuzwa.
(K) Fadhili zako, Ee Bwana, nitaziimba milele.
Maana fahari ya nguvu zao ni Wewe,
Na kwa radhi yako pembe yetu itatukuka.
Maana ngao yetu ina Bwana,
Na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli.
(K) Fadhili zako, Ee Bwana, nitaziimba milele.
Lk 7:16
Aleluya, aleluya,
Nabii mkuu ametokea kwetu, na Mungu amewaambia watu wake.
Aleluya.
Mk 2:1-12
Baada ya siku Yesu akaingia tena Kapernaumu. Ikasikiwa ya kwamba Yesu alikuwa nyumbani. Wakusanyika watu wengi, isibaki nafasi hata mlangoni; akawa akisema nao neno lake. Wakaja watu wakimletea mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne. Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza. Naye Yesu, alipoiona Imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Na baadhi yay a waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao, Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu? Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu? Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza), Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende nyumbani kwako. Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Namna hii hatujapata kuiona kamwe.
Maoni
Ingia utoe maoni