Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Sherehe Ya Epifania (Jumapili, Januari 07, 2024)  

Somo la 1

Isa 60:1-6

Ondoka, ee Yerusalemu, uangaze; Kwa kuwa nuru yako imekuja. Na utukufu wa Bwana umekuzukia. Maana, tazama, giza litaifunika dunia, Na giza kuu litazifunika kabila za watu; Bali Bwana atakuzukia wewe, Na utukufu wake utaonekana juu yako. Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako. Inua macho yako, utazame pande zote; Wote wanakusanyana; wanakujia wewe; Wana wako watakuja kutoka mbali, Na binti zako watabebwa nyongani. Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa utakuwasilia. Wingi wa ngamia utakufunika, Ngamia vijana wa Midiani na Efa; Wote watakuja kutoka Sheba; Wataleta dhahabu na uvumba; Na kuzitangaza sifa za Bwana.

Wimbo wa Katikati

Zab 72:1-2, 7-8, 10-13

Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako.
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu. 
(K) Mataifa yote ya ulimwengu, watakusujudia, ee Bwana.

Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, 
Na wingi wa Amani hata mwezi utakapokoma
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka mto hata miisho ya dunia. 
(K) Mataifa yote ya ulimwengu, watakusujudia, ee Bwana.

Wafalme wa Tarshisi na visiwa walete kodi, 
Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa.
Naam, wafalme wote na wamsujudie;
Na mataifa yote wamtumikie. 
(K) Mataifa yote ya ulimwengu, watakusujudia, ee Bwana.

Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
Na nafsi za wahitaji ataziokoa. 
(K) Mataifa yote ya ulimwengu, watakusujudia, ee Bwana.

Somo la 2

Efe 3:2-3, 5-6

Ndugu zangu: Ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo. Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.

Shangilio

Yn 8:12

Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi nuru ya Ulimwengu, asema Bwana, Yeye anifuataye atakuwa na nuru ya uzima
Aleluya.

Injili

Mt 2:1-12

Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, ansi tumekuja kumsujudia. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao: Kristo azaliwa wapi? Nao wakamwambia, Katika Bethlemu ya Uyahudi; kwa maana ndiyvo ilivyoandikwa na nabii, Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda, Kwa kuwa kwako atatoka mtawala atakayewachunga watu wangu Israeli. Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota, Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie. Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, hata ikaenda ikasimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto. Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.

Maoni


Ingia utoe maoni