Masomo ya Misa
Jumamosi ya Oktava ya Kuzaliwa Bwana (Jumamosi, Desemba 30, 2023)
1Yoh 2:12-17
Nawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu, kwa ajili ya jina lake. Nawaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu. Nimewaandikia ninyi, watoto, kwa sababu mmemjua Baba. Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmeshinda yule mwovu. Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.
Zab 96:7-10
Mpeni Bwana, enyi jamaa za watu,
Mpeni Bwana utukufu na nguvu,
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake.
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie
Leteni sadaka mkaziingie nyua zake,
Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu,
Tetemekeni mbele zake, nchi yote.
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie
Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki;
Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike,
Atawahukumu watu kwa adili.
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie
Shangilio
Aleluya, aleluya
Siku takatifu imetung’aria: Enyi mataifa njoni mkamwabudu Bwana: Kwa sababu mwanga mkubwa umeshuka duniani.
Aleluya.
Lk 2:36-40
Siku ile palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yaliyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya, mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.
Maoni
Ingia utoe maoni