Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Sikukuu ya Watoto Watakatifu Mashahidi (Alhamisi, Desemba 28, 2023)  

Somo la 1

1Yoh 1:5-2:2

Hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala giza lolote hamna ndani yake. Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukizidi ungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu. Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.

Wimbo wa Katikati

Zab 124:1-4, 7-8

Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Israeli na aseme sasa,
Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Wanadamu walipotushambulia.
(K) Nafsi yetu imeokoka kama ndege, katika mtego wa wawindaji.

Papo hapo wangalitumeza hai,
Hasira yao ilipowaka juu yetu;
Papo hapo maji yangalitugharikisha,
Mto ungalipita juu ya roho zetu.
(K) Nafsi yetu imeokoka kama ndege, katika mtego wa wawindaji.

Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.
Msaada wetu u katika jina la Bwana,
Aliyezifanya mbingu nan chi.
(K) Nafsi yetu imeokoka kama ndege, katika mtego wa wawindaji.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Ee Mungu, tunakusifu, tunakukiri kuwa Bwana. Jamii tukufu ya Mitume inakusifu.
Aleluya.

Injili

Mt 2:13-18

Mamajusi walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu. Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliohakikisha kwa wale mamajusi. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti ilisikiwa Rama, kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako.

Maoni


Ingia utoe maoni