Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 3 ya Majilio (Alhamisi, Desemba 21, 2023)  

Somo la 1

Wim 2:8-14

Sikiliza! Ni mpendwa wangu! Tazama, anakuja, Akiruka milimani, akichachawa vilimani. Mpendwa wangu ni kama paa, au ayala. Tazama, asimama nyuma ya ukuta wetu, Achungulia dirishani, atazama kimiani. Mpendwa wangu alinena, akaniambia, Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako, Maana tazama, kaskazi imepita, Masika imekwisha, imekwenda zake; Maua yatokea katika nchi, Wakati wa kupelea umefika, Na sauti ya mwigo husikiwa kwetu. Mtini wapevusha tini zake, Na mizabibu inachanua, Inatoa harufu yake nzuri; Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako. Hua wangu, mafichoni mwa jabali, Katika sitara za magenge, Nitazame uso wako, nisikie sauti yako, Maana sauti yako ni tamu na uso wako mzuri.

Wimbo wa Katikati

Zab 33:2-3, 11-12, 20-21

Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
Mwimbieni wimbo mpya,
Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.
(K) Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki: Mwimbieni wimbo mpya.

Shauri la Bwana lasimama milele,
Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.
Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
(K) Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki: Mwimbieni wimbo mpya.

Nafsi zetu zinamngoja Bwana;
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Maana mioyo yetu itamfurahia,
Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu.
(K) Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki: Mwimbieni wimbo mpya.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Ee Utokaye Mashariki, uliye mng’ao wa mwanga wa milelel na jua la haki, njoo kuwaangazia wakaao gizani na katika kivuli cha mauti.
Aleluya.

Injili

Lk 1:39-45

Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.

Maoni


Ingia utoe maoni