Masomo ya Misa
Ijumaa ya 33 ya Mwaka (Ijumaa, Novemba 24, 2023)
1Mak 4:36-37,52-59
Yuda na ndugu zake walisema, Sasa adui zetu wamevunjwa nguvu, basi tupande tukapatakase mahali patakatifu na kupatabaruku. Jeshi lote likakusanyika likapanda juu ya mlima Sayuni. Wakaondoka mapema siku ya ishirini na tano ya mwezi wa tisa, yaani Kislevu, mwaka mia arobaini na nane, wakatoa dhabihu, kama ilivyoamriwa katika sheria, juu ya madhabahu mpya ya sadaka za kuteketezwa waliyokuwa wameifanya. Wakati ule ule na siku ile ile iliyotiwa unajisi na mataifa, siku ile ile iliwekwa wakfu tena kwa nyimbo na vinubi na vinanda na matari. Watu wote wakaanguka kifudifudi wakipaza sifa kwa mbingu, kwake aliyewapa ufanisi. Wakaiadhimisha sikukuu ya kuitabaruku madhabahu muda wa siku nane, wakileta sadaka za kuteketezwa kwa furaha na kutoa dhabihu ya wokovu na shukrani. Pia, waliupanda ukuta wa mbele wa hekalu kwa taji za dhahabu na vigao; wakaweka wakfu malango na vyumba vya makuhani na kuvitia milango. Kulikuwa na furaha kubwa kwa watu, na aibu iliyoletwa na mataifa iliondolewa. Yuda na ndugu zake, na jamii yote ya Israeli, walikata shauri ya kuwa siku za kuitabaruku madhabahu ziadhimishwe kwa furaha na shangwe kila mwaka kwa wakati wake, muda wa siku nane tangu ishirini na tano ya mwezi Kislevu.
1Nya 29:10-12
Uhimidiwe, Ee Bwana,
Mungu wa Israeli baba yetu,
Milele na milele.
(K) Tulisifu jina lako tukufu, Ee Bwana.
Ee Bwana, ukuu ni wako,
Na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi.
Utajiri na heshima hutoka kwako.
(K) Tulisifu jina lako tukufu, Ee Bwana.
Wewe watawala juu ya vyote,
Na mkononi mwako mna uweza na nguvu,
Tena mkononi mwako mna kuwatukuza,
Na kuwawezesha wote.
(K) Tulisifu jina lako tukufu, Ee Bwana.
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema: Siwaiti tena watumwa, lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.
Lk 19:45-48
Yesu aliingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi. Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza; wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye, wakimsikiliza.
Maoni
Ingia utoe maoni