Masomo ya Misa
Jumatano ya 33 ya Mwaka (Jumatano, Novemba 22, 2023)
2Mak 7:1,20-31
Ilitokea ya kuwa ndugu saba, pamoja na mama yao, walikamatwa kwa amri ya mfalme na kuteswa sana kwa mijeledi na mapigo ili kuwashurutisha kuonja nyama marufuku ya nguruwe. Aliyekuwa wa ajabu hasa, na kustahili kumbukumbu la heshima, ndiye yule mama. Maana aliwaona wanawe saba wakifa kwa siku moja, akistahimili kwa moyo thabiti kwa ajili ya matumaini aliyoyaweka kwa Bwana. Kwa roho hodari aliimarisha tabia yake ya kike kwa ushupavu wa kiume, akamfariji kila mtoto kwa lugha ya wazee wao, akisema, Jinsi mlivyoingia tumboni mwangu sijui. Si mimi niliyekupeni roho na uzima, wala si mimi niliyeziunga sehemu za miili yenu. Bali ni yeye, Muumba ulimwengu; yeye aumbaye wanadamu na kukikusudia chanzo cha vitu vyote; naye kwa rehema zake akakurudishieni roho zenu na uzima wenu, kwa kuwa ninyi sasa mnajihesabu kuwa si kitu kwa ajili ya amri zake. Antioko alijiona anafedheheshwa, lakini bila kuangalia mzaha wa maneno yake, alimsihi yule mdogo, maana alikuwa yungali hai, akamwambia, si kwa maneno tu ila pia kw auapa, ya kuwa, akama ataziacha sheria za wazee wake, atampatia mali nyingi na hali njema; tena, atamfanya mmoja wa rafiki zake na kumkabidhi kazi za ufalme. Yule kijana asipokubali, alimwita mama yake, akamtaka amshawishi mtoto ajiokoe. Akasema naye kwa maneno mengi, hata mwisho alikubali kumshauri mwanawe. Akamwinamia na huku anamdhihaki yule mfalme mkali akasema hivi kwa lugha ya wazee wake: Mwanangu, unirehemu mimi niliyekuchukua tumboni mwangu kwa miezi tisa, na kukutunza na kukulea mpka sasa. Nakusihi, mwanangu, inua macho yako utazame mbingu na nchi, ukaone vitu vyote vilivyomo; fahamu kwamba Mungu hakuviumba kwa vitu vilivyokuwapo. Na ndivyo alivyofanya wanadamu pia. Usiogope mwuaji huyu; jionyeshe umestahilika sawasawa na dnugu zako. Kubali kufa kwako, ili kwa rehema ya Mungu nikupokee tena pamoja na ndugu zako. Hakudiriki kuyamaliza maneno yake, ila yule kijana alisema, Mnamngoja nini? Mimi siitii amri ya mfalme, bali naitii amri ya sheria waliyopewa baba zetu kwa Musa. Wewe, uliyebuni kila namna ya uovu juu ya Waebrania, hutaokoka kabisa katika mikono ya Mungu.
Zab 17:1,5-6,8,15
Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa maombi yangu,
Yasiotoka katika midomo ya hila.
(K) Nishibishe kwa sura yako, Ee Bwana.
Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako,
Hatua zangu hazikuondoshwa.
Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitikia,
Utege sikio lako ulisikie neno langu.
(K) Nishibishe kwa sura yako, Ee Bwana.
Unilinde kama mboni ya jicho,
Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako.
Nikutazame uso wako katika haki,
Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.
(K) Nishibishe kwa sura yako, Ee Bwana.
Yn 10:27
Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.
Lk 19:11–28
Makutano waliposikia, Yesu aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara. Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi. Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja. Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale. Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake. Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi. Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi. Akaja wa pili, akasema, Bwana fungu lako limeleta mafungu matano faida. Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano. Akaja mwingine akasema, Bwana hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso, Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda. Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda; basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake? Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang’anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi. Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi, Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho. Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwanchinje mbele yangu. Na laipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu.
Maoni
Ingia utoe maoni