Jumamosi. 27 Julai. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 32 ya Mwaka (Jumamosi, Novemba 18, 2023)  

Somo la 1

Hek 18:14-16, 19:6-9

Mambo yote yalipokuwa kimya, na usiku ulikuwa katikati ya mwendo wake mwepesi, Neno lako Mwenyezi alishuka mbinguni kutoka kiti chako cha kifalme, shujaa aliye hodari, katika nchi iliyoposishwa hukumu, mwenye upanga mkali, ndio amri yako isiyopindika, akasimama na kujaza mambo yote mauti, na pindi alipogusa mbingu akaikanyaga nchi. Kwa maana ulimwengu mzima, kwa kadiri ya asili yake, ulifanyika tena mpya, kwa kuzitii amri zako hizi na hizi, ili watoto wako walindwe wasipate dhara. Uwingu ulionekana uliokitia uvuli kituo chao, nan chi kavu ikapanda kutoka pale palipokuwapo maji kwanza, katika Bahari ya Shamu kukawa barabara isiyo na zuio, na uwanda wenye majani katika mawimbi yaumkayo. Hapo watu wako wakapita pamoja na majeshi yao yote, ambao kwa mkono wako walifunikwa, wakiisha kuona maajabu makuu. Wakazunguka-zunguka huru kama farasi, wakaruka-ruka kama wana-kondoo, wakikuhimidi Wewe, Bwana, uliyekuwa mkombozi wao.

Wimbo wa Katikati

Zab 105:2-3, 36-37, 42, 43

Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
(K) Zikumbukeni ajabu Bwana alizozifanya.

Akawapiga wazaliwa wa kwanza katika nchi.
Malimbuko ya nguvu zao.
Akawatoa hali wana fedha na dhahabu,
Katika kabila zao asiwepo mwenye kukwaa.
(K) Zikumbukeni ajabu Bwana alizozifanya.

Maana alilikumbuka neno lake takatifu,
Na Ibrahimu, mtumishi wake.
Akawatoa watu wake kwa shangwe,
Na wateule wake kwa nyimbo za furaha.
(K) Zikumbukeni ajabu Bwana alizozifanya.

Shangilio

Zab 119:105

Aleluya, aleluya,
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya.

Injili

Lk 18:1-8

Yesu aliwaambia wanafunzi wake mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji Fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona Imani duniani?

Maoni


Ingia utoe maoni