Jumatano. 04 Desemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 32 ya Mwaka (Alhamisi, Novemba 16, 2023)  

Somo la 1

Hek 7:22-8:1

Mradi ndani yake mna roho ya welekevu, takatifu, ya pekee, yenye namna mbalimbali, iliyoerevuka, nyepesi kuenea, Dhahiri kusema, safi, wazi, isiyoharibika, ya kupenda wema, hodari, bila kuzuiwa, yenye ukarimu, ya kupenda wanadamu, thabiti, amini, bila mashaka, yenye nguvu, yenye kuangalia mambo yote, na kuingiliana na roho zote zilizo na welekevu, zilizo safi, zilizoerevuka sana. Kwa sababu Hekima huenda upesi kila upande hata kupita mwendo wowote, naam, huenea kote kote katika mambo yote na kupenya ndani yake kwa ajili ya usafi wake. Maana ndiyo pumzi ya uwezo wa Mungu, na miminiko nakawa la utukufu wake Mwenyezi, hivyo lolote lililo najisi haliwezi kuingia ndani yake. Ndiyo mwangaza kutoka kwa nuru ya milele, na kioo kisicho na mawaa cha kutenda kwake Mungu, na mfano wa wema wake. Nayo ni moja, ina uwezo wa kutenda yote; hujikalia, huweza kuhuisha yote; na tangu kizazi hata kizazi huwaingilia roho takatifu, huwafanya wanadamu kuwa rafiki za Mungu na manabii; maana Mungu humpenda yeye tu akaaye na Hekima. Marini kuliko jua. Hekima hupita makundi ya nyota; ikilinganishwa na nuru, huonekana ya kuwa imezidi; mradi baada ya nuru ya mchana hufuata usiku, bali juu ya Hekima hakuna ovu liishindalo. Hekima huenea kwa nguvu nyingi toka pembe hii hata pembe hii ya dunia, na kuyaratibisha mambo yote kwa jinsi ya kufaa.

Wimbo wa Katikati

Zab 119:89-91,130,135,175

Ee Bwana, neno lako lasimama,
Imara mbinguni hata milele.
Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi.
Umeiweka nchi, nayo inakaa.
(K) Ee Bwana, neno lako lasimama hata milele.

Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo,
Maana vitu vyote ni watumishi wako.
Kufafanusha maneno yako kwatia nuru,
Na kumfahamisha mjinga. 
(K) Ee Bwana, neno lako lasimama hata milele.

Umwangazie mtumishi wako uso wako,
Na kunifundisha amri zako.
Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu,
Na hukumu zako zinisaidie. 
(K) Ee Bwana, neno lako lasimama hata milele.

Shangilio

Zab 119:135

Aleluya, aleluya,
Umwangazie mtumishi wako uso wako, na kunifundisha amri zako.
Aleluya.

Injili

Lk 17:20-25

Yesu alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, Ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu. Akawaambia wanafunzi, Siku zitakuja mtakapotamani kuona siku moja katika siku zake Mwana wa Adamu, msiione. Tena watawaambia, Tazama, kule! Tazama, huku! Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate; kwa kuwa, kama vile umeme umulikavyo toka upande huu chini ya mbingu hata upande huu chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake. Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki.

Maoni


Ingia utoe maoni