Masomo ya Misa
Dominika ya 32 ya Mwaka (Jumapili, Novemba 12, 2023)
Hek 6:12-16
Hekima hung’aa, wala hafifii; Huonekana upesi nao wampendao; Hupatikana nao wamtafutao. Hutangulia kujionyesha kwao wamtakao, Amtafutaye mapema hana kazi ngumu; Atamkuta ameketi mlangoni pake. Kumtia fikirani ni ufahamu mkamilifu; Naye mwenye kukesha kwa ajili yake Atakuwa mara hana masumbufu. Yeye huzunguka-zunguka mwenyewe, Akiwatafuta wao wanaomstahili; Njiani hujidhihirisha kwao kwa upendo, Hukutana nao katika kila kusudi.
Zab 63:1-7
Ee Mungu, Mungu wangu nitakutafuta mapema,
Nafsi yangu inakuonea kiu.
Mwili wangu wakuonea shauku,
Katika nchi kama na uchovu, isiyo na maji.
(K) Ee Mungu, Mungu wangu, nafsi yangu inakuonea kiu.
Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu,
Nizione nguvu zako na utukufu wako.
Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai,
Midomo yangu itakusifu.
(K) Ee Mungu, Mungu wangu, nafsi yangu inakuonea kiu.
Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai,
Kwa jina lako nitainua mikono yangu.
Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono,
Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha.
(K) Ee Mungu, Mungu wangu, nafsi yangu inakuonea kiu.
Ninapokukumbuka kitandani mwangu,
Nakutafakari Wewe makesha yote ya usiku.
Maana Wewe umekuwa msaada wangu,
Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia.
(K) Ee Mungu, Mungu wangu, nafsi yangu inakuonea kiu.
1Thes 4:13-18
Ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo.
Yn 14:23
Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake.
Aleluya.
Mt 25:1-13
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara. Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi, tokeni mwende kumlaki. Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazingeneza taa zo. Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika. Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie. Na hao waliokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa. Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie. Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi. Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.
Maoni
Ingia utoe maoni