Jumatano. 06 Desemba. 2023

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 31 ya Mwaka (Jumamosi, Novemba 11, 2023)  

Somo la 1

Rum 16:3-9, 16, 22-27

Nisalimieni Priska na Akila, watenda kazi pamoja nami katika Kristo Yesu; waliokuwa tayari hata kukatwa kichwa kwa ajili ya maisha yangu ambao ninawashukuru, wala si mimi tu, ila na makanisa ya Mataifa yote pia; nisalimieni na kanisa lililomo katika nyumba yao. Nisalimieni Epaineto, mpenzi wangu, aliye malimbuko ya Asia kwa Kristo. Nisalimieni Mariamu, aliyejitaabisha sana kwa ajili yenu. Nisalimieni Androniko na Yunia, jamaa zangu, waliofungwa pamoja nami, ambao ni maarufu miongoni mwa mitume; nao walikuwa katika Kristo kabla yangu. Nisalimieni Ampliato, mpenzi wangu katika Bwana. Nisalimieni Urbano, mtenda kazi pamoja nami katika Kristo, na Stakisi, mpenzi wangu. Salimianeni kwa busu takatifu. Makanisa yote ya Kristo wawasalimu. Mimi Tertio, niliyandika waraka huu, nawasalimu katika Bwana. Gayo, mwenyeji wangu na wa Kanisa lote pia awasalimu. Erasto, wakili wa mji, awasalimu, na Kwarto, ndugu yetu. Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo na ile amri iliyositirika tangu zamani za milele, ikadhihirishwa wakati huu kwa maandiko ya manabii ikajulikana na mataifa yote kama alivyowaamuru Mungu wa milele, ili waitii Imani. Ndiye Mungu mwenye hekima peke yake. Utukufu una yeye kwa Yesu Kriso, milele na milele. Amina.

Wimbo wa Katikati

Zab 145:2-5, 10-11

Kila siku nitakuhimidi,

Nitalisifu jina lako milele na milele.
Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana,
Wala ukuu wake hautambulikani.
(K) Nitalihimidi jina lako milele, Ee Bwana.

Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yake,
Kitayatangaza matendo yake makuu.
Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako,
Na matendo yako yote ya ajabu.
(K) Nitalihimidi jina lako milele, Ee Bwana.

Ee Bwana, kazi zako zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako.
(K) Nitalihimidi jina lako milele, Ee Bwana.

Shangilio

Yn 17:17

Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya.

Injili

Lk 16:9-15

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele. Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. Bali, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli? Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe? Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu au kumpenda huyu, ama atamshikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.

Maoni

Vicklina Ponela

Tafakali ya neno

Ingia utoe maoni