Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Sikukuu ya Kutabarukiwa Basilika la Laterani (Alhamisi, Novemba 09, 2023)  

Somo la 1

Eze 43:1-2, 4-7

Malaika alinileta mpaka langoni, yaani, lango lile lielekealo upande wa mashariki; na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling’aa kwa utukufu wake. Na huo utukufu wa Bwana ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile lielekealo upande wa mashariki. Kisha Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa Bwana uliijaza nyumba. Nikasikia sauti ya mmoja asemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo; na mtu akasimama karibu nami. Akaniambia, Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele.

Wimbo wa Katikati

Zab 122:1-5, 7-8

Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.
(K)Nalifurahi waliponiambia,na twende nyumbani kwa Bwana.

Ee Yerusalemu uliyejengwa Kama mji ulioshikamana,
Huko ndiko walikopanda kabila, Kabila za Bwana;
Ushuhuda kwa Israeli, Walishukuru jina la Bwana.
(K)Nalifurahi waliponiambia,na twende nyumbani kwa Bwana.

Maana huko viliwekwa viti vya hukumu, Viti vya enzi vya mbari ya Daudi.
Amani na ikae ndani ya kuta zako, Na kufanikiwa ndani ya majumba yako.
Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu Niseme sasa, Amani ikae nawe.
(K)Nalifurahi waliponiambia,na twende nyumbani kwa Bwana.

Somo la 2

1Kor 3:9-11, 16-17

Ninyi ni jingo la Mungu. Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, yesu Kristo. Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani, au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa Dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, nay a kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.

Shangilio

2Nya 7:16

Aleluya, aleluya,
Nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, asema Bwana, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele.
Aleluya.

Injili

Yn 2:13-22

Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu alikwea mpaka Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara. Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila. Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuonyeshayo, kwamba unafanya haya? Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, name katika siku t atu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake. Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu.

Maoni


Ingia utoe maoni