Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Sikukuuu ya Marehemu Wote (Jumatano, Novemba 02, 2016)  

Somo la 1

Isa 25:6-9

Na katika mlima huu Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana. Naye katika mlima huu atauharibu uso wa sitara iliyowekwa juu ya watu wote, na utaji ule uliotandwa juu ya mataifa yote. Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo. Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake.

Wimbo wa Katikati

Zab 27:1, 4, 7-9,13-14

Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu,
Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu ninalia, Unifadhili, unijibu.
Uliposema, Nitafuteni uso wangu, Moyo wangu umekuambia,
Bwana, uso wako nitautafuta.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira.
Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

Somo la 2

Rum 5:5-11

Tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho.

Shangilio

Ufu. 14:13

Aleluya, aleluya,
Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa! Wapate kupumzika baada ya taabu zao, kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.
Aleluya.

Injili

Lk 7:11-17

Yesu alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando.

Maoni


Ingia utoe maoni