Masomo ya Misa
Alhamisi ya 26 ya Mwaka (Alhamisi, Oktoba 05, 2023)
Neh 8:1-12
Watu wote walikusanyika kama mtu mmoja katika uwanja uliokuwa mbele ya lango la maji; wakamwambia Ezra, mwandishi, akilete kitabu cha torati ya Musa, Bwana aliyowaamuru Israeli. Naye Ezra, kuhani, akaileta torati mbele ya kusanyiko, la wanaume na wanawake, na wote walioweza kusikia na kufahamu, siku ya kwanza na mwezi wa saba. Akasoma humo mbele ya uwanja uliokuwa ukikabili lango la maji, tangu mapambazuko hata adhuhuri, mbele ya hao wanaume na wanawake, na wale walioweza kufahamu; na masikio ya watu wote yakasikiliza kitabu cha torati. Naye Ezra, kuhani, akasimama juu ya mimbari ya mti, waliyokuwa wameifanya kwa kusudi hilo; na karibu naye wakasimama Matithia, na Shema, na Anaya, na Uria, na Hilkia, na Maaseya, mkono wake wa kuume; na mkono wake wa kushoto, Pedaya, na Misbaeli, na Malkiya, na Hashumu, na Hashbadani, na Zekaria, na Meshulamu. Ezra akakifunua kitabu machoni pa watu wote; (maana alikuwa juu ya watu wote); na hapo alipokifungua, watu wote walisimama; Ezra akamhimidi Bwana, Mungu Mkuu. Nao watu wote wakaitika, Amina, Amina, pamoja na kuinua mikono yao; kisha wakainama vichwa vyao, wakamsujudu Bwana kifudifudi. Tena Yeshua, na Bani, na Sherebia, na Yamini, na Akubu, na Shabethai, na Hodai, na Maaseya, na Kelita, na Azaria, na Yozabadi, na Hanani, na Pelaya, nao ni Walawi, wakawafahamisha watu torati; na watu wakasimama mahali pao. Nao wakasoma katika kitabu, katika torati ya Mungu, kwa sauti ya kusikilika; wakaeleza maana yake, hata wakayafahamu yaliyosomwa.
Zab 19:7-10
Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima.
(K) Amri ya Bwana huufurahisha moyo.
Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia macho nuru.
(K) Amri ya Bwana huufurahisha moyo.
Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa.
(K) Amri ya Bwana huufurahisha moyo.
Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
Kuliko wingi wa dhahabu safi.
Nazo ni tamu kuliko asali,
Kuliko sega la asali.
(K) Amri ya Bwana huufurahisha moyo.
Mt 11:25
Aleluya, aleluya,
Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya.
Lk 10:1-12
Bwana aliweka wafuasi wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni, angalieni, nawatuma kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu. Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie mtu njiani. Na nyumba yo yote mtakayoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihame-hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii. Na mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; waponyeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia. Na mji wo wote mtakaouingia, nao hawawakaribishi, tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni, Hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana na miguu yetu tunayakung'uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia. Nawaambia ya kwamba siku ile itakuwa rahisi zaidi Sodoma kuistahimili adhabu yake kuliko mji huo.
Maoni
Ingia utoe maoni