Masomo ya Misa
Jumatatu ya 25 ya Mwaka (Jumatatu, Septemba 25, 2023)
Ezr 1:1-6
Ilikuwa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalame wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, Bwana akamwambia roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia akisema, Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi: Bwana Mungu wa mbinguni amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Mungu wake na awe pamoja naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda, akaijenge nyumba ya Bwana, Mungu wa Israeli, (yeye ndiye Mungu), iliyoko Yerusalemu. Na mtu awaye yote aliyesalia mahali popote akaapo hali ya ugeni, na asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali, na wanyama, zaidi ya vitu vitolewavyo kwa hiari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu. Ndipo wakaondoka wakuu wa mbari za mababa, wa Yuda na Benyamini, na makuhani, na Walawi, naam, watu wote ambao Mungu amewaamsha roho zao kukwea, ili kuijenga nyumba ya Bwana, iliyoko Yerusalemu. Na watu wote, waliokaa karibu nao pande zote wakawatia nguvu mikono yao, kwa vyombo vya fedha, kwa dhahabu, kwa mali, na kwa wanyama, na vitu vya thamani, zaidi ya vile vilivyotolewa kwa hiari ya mtu.
Zab 126
Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
Na ulimi wetu kelele za furaha.
Ndipo waliposema katika mataifa,
“Bwana amewatendea mambo makuu”.
(K) Bwana alitutendea mambo makuu.
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi.
Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini.
(K) Bwana alitutendea mambo makuu.
Wapandao kwa machozi
Watavuna kwa kelele za furaha.
Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda,
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Aichukuapo miganda yake.
(K) Bwana alitutendea mambo makuu.
Yak 1:18
Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya.
Lk 8:16–18
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka uvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake. Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana na kutokea wazi. Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.
Maoni
Ingia utoe maoni