Masomo ya Misa
Ijumaa ya 24 ya Mwaka (Ijumaa, Septemba 22, 2023)
1Tim 6:2-12
Mambo hayo uyafundishe na kuonya. Mtu awaye yote akifundisha elimu nyingine, wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo, wala mafundisho yapatanayo na utauwa, amejivuna; wala hafahamu neno lolote; bali ana wazimu wa kuwazia habari za maswali, na mashindano ya maneno, ambayo katika hayo hutoka husuda, na ugomvi, na matukano, na shuku mbaya; na majadiliano ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida. Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi. Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, Imani, upendo, saburi, upole. Piga vita vile vizuri vya Imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi.
Zab 49:5-9, 16-19
Kwa nini niogope siku za uovu,
Ubaya ukinizunguka miguuni pangu?
Wa hao wanaozitumainia mali zao,
Na kujisifia wingi wa utajiri wao.
(K) Heri walio maskini war oho, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake,
Wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake,
Maana fidia ya nafsi zao ina gharama,
Wala hana budi kuiacha hata milele.
Ili ishi sikuzote asilione kaburi.
(K) Heri walio maskini war oho, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Usiogope mtu atakapopata utajiri
Na fahari ya nyumba yake itakapozidi.
Maana atakapokufa hatachukua chochote;
Utukufu wake hautashuka ukimfuata.
(K) Heri walio maskini war oho, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai,
Na watu watakusifu ukijitendea mema,
Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake,
Hawataona nuru hata milele.
(K) Heri walio maskini war oho, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Zab 19:8
Aleluya, aleluya,
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya.
Lk 8:1–3
Yesu alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yohana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.
Maoni
Ingia utoe maoni