Masomo ya Misa
Jumanne ya 24 ya Mwaka (Jumanne, Septemba 19, 2023)
1 Tim 3: 1-13
Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi. Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi. Vivyo hivyo mashemasi na wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, si watu wa kutumia mvinyo sana,si watu wanaotamani fedha ya aibu. wakiishika siri ya imani katika dhamiri safi. Hawa pia na wajaribiwe kwanza; baadaye waitende kazi ya shemasi, wakiisha kuonekana kuwa hawana hatia. Vivyo hivyo wake zao na wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote. Mashemasi na wawe waume wa mke mmoja, wakiwasimamia watoto wao vizuri, na nyumba zao. Kwa maana watendao vema kazi ya shemasi hujipatia daraja nzuri, na ujasiri mwingi katika imani iliyo katika Kristo Yesu.
Zab 100: 1-3, 5-6
Rehema na hukumu nitaziimba,
Ee Bwana, nitakuimbia zaburi.
Nitaiangalia njia ya unyofu;
Utakuja kwangu lini?
(K) Nitakwenda kwa unyofu wa moyo
Nitakwenda kwa unyofu wa moyo
Ndani ya nyumba yangu.
Sitaweka mbele ya macho yangu
Neno la uovu.
(K) Nitakwenda kwa unyofu wa moyo
Amsingiziaye jirani yake kwa siri,
Huyo nitamharibu.
Mwenye macho ya kiburi na moyo wa majivuno,
Huyo sitavumilia naye.
(K) Nitakwenda kwa unyofu wa moyo
Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi,
Hao wakae nami.
Yeye aendaye katika njia kamilifu,
Ndiye atakayenitumikia.
(K) Nitakwenda kwa unyofu wa moyo
Lk 7:16
Aleluya, aleluya,
Nabii mkuu ametokea kwetu; na Mungu amewaangalia watu wake.
Aleluya.
Lk 7:11-17
Yesu alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando.
Maoni
Ingia utoe maoni