Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 23 ya Mwaka (Ijumaa, Septemba 15, 2023)  

Somo la 1

1 Tim 1:1-2, 12-14

Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu, taraja letu; kwa Timotheo, mwanangu hasa katika imani. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake;ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani. Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu.

Wimbo wa Katikati

Zab 16:1-2, 5, 7-8, 11

Mungu, unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu;
Sina wema ila utokao kwako.
Bwana ndiye fungu la posho langu,
Na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura yangu.
(K) Bwana ndiye fungu la posho langu.

Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.
(K) Bwana ndiye fungu la posho langu.

Utanijulisha njia ya uzima;
Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele.
(K) Bwana ndiye fungu la posho langu.

Injili

Lk 6:39-42

Yesu aliwaambia wanafunzi wake mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili? Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.

Maoni


Ingia utoe maoni