Ijumaa. 17 Mei. 2024

Masomo ya Misa

ALHAMISI JUMA LA 1 LA KWARESIMA (Alhamisi, Februari 18, 2016)  

Somo la 1

Est. 4:1-14

Malkia Esta naye alimkimbilia Bwana, akishikwa na uchungu wa mauti. Akazivua nguo zake za fahari akavaa nguo za huzuni, na kilio, na badala ya manukato mazuri alijitia majivu na samadi kichwani; akajinyenyekesha mwili wake, hata mahali pa mapambo ya furaha alijifunika kwa nywele zake zilizofumuliwa. Akamwomba Bwana wa Israeli, akisema: Bwana wangu, Wewe peke yako u Mfalme wetu. Unisaidie mimi niliye mkiwa, wala sina msaidizi wmingine ila Wewe; maana hatari yangu imo mkononi mwangu. Tangu nilipozaliwa katika kabila ya jamaa yangu, nimesikia ya kuwa Wewe, Bwana, ulimchagua Israeli katika mataifa yote, na baba zetu katika jamaa zao, kuwa urithi wa daima, ukawatimilizia yote uliyoyaahidi. Utukumbuke, Ee Bwana; ujifunue wakati wa taabu yetu; unipe moyo thabiti, Ee Mfalme wa miungu na Bwana wa milki zote. Unitie kinywani mwangu maneno ya kufaa mbele ya samba, ukaugeuza moyo wake apate kumchukia yule anayepigana nasi, ili akomeshwe pamoja na wote wenye nia moja naye. Lakini utuokoe sisi kwa mkono wako; unisaidie mimi niliye peke yangu, bila msaidizi mwingine ila Wewe, Bwana.

Wimbo wa Katikati

Zab. 138:1-3, 8-9 (K) 1

(K) Siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.

Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu,
Nitalishukuru jina lako. (K)

Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
Kwa amana umeikuza ahadi yako,
Kuliko jina lako lote.
Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)

Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
Bwana atanitimilizia mambo yangu;
Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
Usiziache kazi za mikono yako. (K)

Injili

Mt. 7:7-12

Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akiomwomba mkate, atampa jiwe? Atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao? Basi yoyote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hivyo ndiyo torati na manabii.

Maoni


Ingia utoe maoni