Masomo ya Misa
Jumanne ya 20 ya Mwaka (Jumanne, Agosti 22, 2023)
Amu 6:11-24
Malaika wa Bwana akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani. Malaika wa Bwana akamtokea, akamwambia, Bwana yu pamoja nawe, Ee shujaa. Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye Bwana, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. Bwana akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma? Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu. Bwana akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja. Naye akamwambia, Kama nimepata kibali mbele za macho yako, basi unionyeshe ishara, ya kuwa ndiwe wewe unayesema nami. Tafadhali, usiondoke hapa hata nikujie, nikatoe zawadi yangu, na kuiweka mbele zako. Akasema, Nitangoja hata utakaporudi. Basi Gideoni akaingia ndani, akaandaa mwana-mbuzi, na mikate isiyotiwa chachu, ya efa ya unga; akaitia ile nyama katika kikapu, akautia mchuzi katika nyungu, akamletea hapo nje chini ya mwaloni, akampa. Naye malaika wa Mungu akamwambia, Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uiweke juu ya mwamba huu, ukaumwage huu mchuzi. Akafanya hivyo. Ndipo malaika wa Bwana akanyosha ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwake, akaigusa ile nyama na ile mikate; moto ukatoka mwambani, ukaiteketeza ile nyama na mikate; malaika wa Bwana akaondoka mbele ya macho yake. Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa Bwana; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona Bwana uso kwa uso. Bwana akamwambia Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa. Ndipo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri.
Zab 85:8, 10-13
Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawaambia watu wake amani,
Naam, na watauwa wake pia,
Bali wasiurudie upumbavu tena.
(K) Bwana atawaambia watu wake amani.
Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na amani zimehusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni.
(K) Bwana atawaambia watu wake amani.
Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.
(K) Bwana atawaambia watu wake amani.
Mt 19:23-30
Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Wanafunzi waliposikia, walishangaa mno, wakisema, Ni nani basi awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akawaambia, Kwa wanadamu hilo haliwezekani; bali kwa Mungu yote yawezekana. Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi? Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele. Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.
Maoni
Ingia utoe maoni