Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni. (Jumanne, Agosti 15, 2023)  

Somo la 1

Ufu 11: 19, 12: 1-6, 10

Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake. Kukawa na umeme, na sauti, na radi, na tetemeko la nchi, na mnua ya mawe nyingi sana. Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili. Naye alikuwa ana mimba, akilia, hali ana utungu na kuumwa katika kuzaa. Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba. Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za muinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake. Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi. Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambapo ana mahali palipotengenezwa na Mungu, ili wamlishe huko muda wa siku elfu na mia mbili na sitini. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.

Wimbo wa Katikati

Zab. 45: 9-11, 15

Binti za wafalme wamo
Miongoni mwa akina bibi wako wastahiki.
Mkono wako wa kuume amesimama malkia,
Amevaa dhahabu ya Ofiri.
Sikia, binti, utazame, utege sikio lako,
Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako.
(K) Mkono wako wa kuume amesimama malkia. amevaa dhahabu ya Ofiri.

Naye mfalme atautamani uzuri wako,
Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie.
Watapelekwa kwa furaha na shangwe,
Na kuingia katika nvumba va mfalme.
(K) Mkono wako wa kuume amesimama malkia. amevaa dhahabu ya Ofiri.

Somo la 2

1Kor 15: 20-26

Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watanuishwa. Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja. Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu. Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Maria amepalizwa mbinguni majeshi yote ya malaika wanafurahi.
Aleluya.

Injili

Lk 1: 39-56

Mariamu aliondoka, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeth Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana. Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu. Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi Kwa hao wanaomcha. Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha mema Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele. Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.

Maoni


Ingia utoe maoni