Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 13 ya Mwaka (Ijumaa, Julai 07, 2023)  

Somo la 1

Mwa 23:1-4, 19; 24:1-8, 62-67

Umri wake Sara ulikuwa miaka mia na ishirini na saba, ndio umri wake Sara. Sara akafa katika Kiriath-arba, ndio Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Ibrahimu akaja kumlilia Sara na kumwombolezea. Akaondoka Ibrahimu kutoka mbele ya maiti wake, akasema na bani Hethi, akinena, Mimi ni mgeni, ninatembea kwenu; nipeni mahali pa kuzikia kwenu, pawe pangu, nimzike maiti wangu atoke mbele yangu. Basi baada ya hayo Ibrahimu akamzika Sara mkewe katika pango ya shamba la Makpela kuelekea Mamre, ndiyo Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na Bwana alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote. Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, nami nitakuapisha kwa Bwana, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao; bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke. Yule mtumishi akamwambia, Labda yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii, Ibrahimu akamwambia, Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko. Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babaangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, anwe utamtwalia mwanangu mke tokea huko; na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko. Basi isaka alikuwa amekuja kwa njia ya Beer-lahai-roi, maana laikaa katika nchi ya kusini. Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja. Rebeka akainua macho, anaye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia. Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika. Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda. Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamaake.

Wimbo wa Katikati

Zab 106:1-5

Aleluya.
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
kwa maana fadhili zake ni za milele.
Nani awezaye kuyanena matendo makuu ya Bwana,
kuzihubiri sifa zake zote.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.

Heri washikao hukumu,
Na kutenda haki sikuzote.
Ee Bwana, unikumbuke mimi,
Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.

Unijilie kwa wokovu wako,
Ili niuone wema wa wateule wako.
Nipate kuifurahia furaha ya taifa lako,
Na kujisifu pamoja na watu wako.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.

Shangilio

Zab 130:5

Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja Bwana, na Neno lake nimelitumainia.
Aleluya.

Injili

Mt 9:9–13

Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata. Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.

Maoni


Ingia utoe maoni