Masomo ya Misa
Ijumaa ya 29 ya Mwaka (Ijumaa, Oktoba 21, 2016)
Efe 4:1-6
Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.
Zab 24:1-6
Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari, Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
(K) Hiki ndicho kizazi cha wakufuatao, Ee Bwana.
Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili
(K) Hiki ndicho kizazi cha wakufuatao, Ee Bwana.
Atapokea baraka kwa Bwana, Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao, Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo.
(K) Hiki ndicho kizazi cha wakufuatao, Ee Bwana.
Efe. 1:17, 18
Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya.
Lk 12:54-59
Yesu aliwaambia makutano pia, kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo. Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya? Na mbona ninyi wenyewe kwa nafsi zenu hamwamui yaliyo haki? Maana, unapofuatana na mshitaki wako kwenda kwa mwamuzi, hapo njiani fanya bidii kupatanishwa naye, asije akakuburuta mpaka mbele ya kadhi; yule kadhi akakutia mikononi mwake mwenye kulipiza, na yule mwenye kulipiza akakutupa gerezani. Nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.
Maoni
Ingia utoe maoni