Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 29 ya Mwaka (Alhamisi, Oktoba 20, 2016)  

Somo la 1

Efe 3:14-21

Nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa, awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu. Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina.

Wimbo wa Katikati

Zab 33:1-2, 4-5, 11-12, 18-19

Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
Mshukuruni Bwana kwa kinubi, Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
(K) Nchi imejaa fadhili za bwana.

Kwa kuwa neno la Bwana lina adili, Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu, Nchi imejaa fadhili za Bwana.
(K) Nchi imejaa fadhili za bwana.

Shauri la Bwana lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.
Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
(K) Nchi imejaa fadhili za bwana.

Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa.
(K) Nchi imejaa fadhili za bwana.

Shangilio

Yn. 17: 17

Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya.

Injili

Lk 12:49-53

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi? Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe! Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano. Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu. Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu.

Maoni


Ingia utoe maoni