Masomo ya Misa
Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu (Ijumaa, Juni 16, 2023)
Kum 7:6-11
Musa aliwaambia makutano: Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana Mungu wako; Bwana, Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi. Bwana hakuwapenda ninyi, wala hakuwachagua ninyi, kwa sababu mlikuwa wengi kuliko mataifa yote, maana mlikuwa wachache kuliko watu wote; bali kwa sababu Bwana anawapenda, na kwa sababu alitaka kuutimiza uapo wake aliowaapia baba zenu, ndiyo sababu Bwana akawatoa kwa mkono wa nguvu, akawakomboa katika nyumba ya utumwa katika mkono wa Farao, mfalme wa Misri. Basi, jueni ya kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu; naye huwalipa wamchukiao mbele ya uso wao, ili kuwangamiza. Hatakuwa mlegevu kwake yeye amchukiaye, atamlipa mbele ya uso wake. Basi zishike amri, na sheria, na hukumu ninazoamuru leo, uzitende.
Zab 103:1–4, 6–8, 10
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Fadhili za Bwana zina wamchao, tangu milele hata milele.
Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema.
(K) Fadhili za Bwana zina wamchao, tangu milele hata milele.
Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki,
Na hukumu kwa wote wanaoonewa.
Alimjulisha Musa njia zake,
Wana wa Israeli matendo yake.
(K) Fadhili za Bwana zina wamchao, tangu milele hata milele.
Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Hakututenda sawasawa na hatia zetu,
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.
(K) Fadhili za Bwana zina wamchao, tangu milele hata milele.
1Yoh 4:7–16
Wapenzi na tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu. Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu. Katika hili tunafahamu ya kuwa tunakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa kuwa ametushirikisha Roho wake. Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa Baba amemtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu. Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu. Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.
Mt 11:29
Aleluya, aleluya,
Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.
Aleluya.
Mt 11:25-30
Wakati ule Yesu alijibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndiyvo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia. Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.
Maoni
Ingia utoe maoni