Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 10 y Mwaka (Jumatatu, Juni 12, 2023)  

Somo la 1

2Kor 1:1-7

Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu; kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, pamoja na watakatifu wote walioko katika nchi yote ya Akaya. Neema na iwe kwenu na Amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote; atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu. Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo. Lakini ikiwa sisi tu katika dhiki, ni kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu; au ikiwa twafarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu; ambayo hutenda kazi yake kwa kustahimili mateso yale tuteswayo na sisi. Na tumaini letu kwa ajili yenu ni imara, tukijua ya kuwa kama vile mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo mmekuwa washiriki wa zile faraja.

Wimbo wa Katikati

Zab 34:1 – 8

Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema

Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote.
(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema

Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote.
(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema

Malaika wa Bwana hufanya kituo,
Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema;
Heri mtu yule anayemtumaini.
(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema

Shangilio

Zab 119:18

Aleluya, aleluya,
Unifumbue macho yangu niyatazame, maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.

Injili

Mt 5: 1-12

Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, Heri walio maskini war oho; maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; maana hao watafarijika. Heri wenye upole; maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema; maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.

Maoni


Ingia utoe maoni