Masomo ya Misa
Jumamosi ya 9 ya Mwaka (Jumamosi, Juni 10, 2023)
Tob. 12:1, 5-15, 20
Karamu ilipokwisha Tobiti akamwita mwanawe Toba, akamwambia, Mwanangu, angalia mtu huyu aliyefuatana nawe alipwe mshahara wake, na lazima uongeze. Basi akamwita malaika, akamwambia, Afadhali sana wewe utwae nusu ya yote mliyoleta. Ndipo alipowachukua wote wawili kwa faragha na kumwadhimisha; na kumpa shukrani mbele ya wote walio hai kwa mambo yote aliyowatendeeni. Ni vema kumhimidi Mungu, na kulikuza jina lake; na kuyatangaza kwa heshima matendo ya Mungu. Basi msilegee katika kumshukuru. Ni vema kuisetiri siri ya mfalme, bali kuyafunua kwa utukufu matendo ya Mungu. Mtende yaliyo mema, na mabaya hayatawapata. Bora ni kusali pamoja na kufunga na kutoa sadaka za haki. Kidogo pamoja na haki ni bora kuliko wingi pasipo na haki. Yafaa kutoa sadaka kuliko kuweka akiba ya dhahabu. Sadaka huokoa na mauti, nazo zitasafishia mbali dhambi zote. Watoao sadaka na kutenda haki watajaa uzima, bali watendao dhambi ni adui za uhai wao wenyewe. Hakika sitawaficheni neno. Nimesema, Ni vema kuisetiri siri ya mfalme, bali kuyafunua kwa utukufu matendo ya Mungu. Basi hapo mliposali, wewe na mkweo Sara, mimi naliupeleka ukumbusho wa sala zenu mbele zake Aliye Mtakatifu; na hapo ulipowazika wafu, nalikuwapo pamoja nawe vile vile. Na hapo usipokawia kuondoka na kuacha chakula chako, ili uende kumzika yule mfu, tendo lako jema halikufichwa kwangu; lakini nalikuwapo pamoja nawe. Na sasa Mungu amenituma ili niwaponye, wewe na mkweo Sara. Mimi ndimi Rafaeli, mmojawapo wa malaika watakatifu saba, wapelekao sala za watakatifu, na kuingia mbele za utukufu wake Aliye Mtakatifu. Sasa mshukuruni Mungu; kwa kuwa mimi ninapaa kwake aliyenituma; nanyi andikeni katika kitabu mambo yote yaliyotendeka. Nao walipoondoka hawakumwona tena.
Tob. 13:2, 6
Hurudi, na kurehemu tena,
Hushusha hata kuzimu, na kuinua tena;
Wala hakuna awezaye kujiepusha na mkono wake.
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.
Mkimgeukia kwa moyo wote na roho yote,
Na kutenda kweli zake.
Ndipo atakapowageukia ninyi,
Wala hatawaficheni uso wake.
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.
Angalieni atakavyowatendea:
Mshukuruni kwa vinywa vyenu vyote;
Mhimidini Bwana mwenye haki;
Mtukuzeni Mfalme wa milele.
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.
Katika nchi ya kufungwa kwangu namshukuru;
Nawahubiri taifa la wakosaji nguvu zake na enzi yake.
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.
Enyi wakosaji, geukeni, mkatende haki mbele zake;
Nani ajuaye kama atawakubali na kuwarehemu?
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.
Yn. 10: 27
Aleluya, aleluya.
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.
Mk. 12:38-44
Yesu aliwaambia katika mafundisho yake: Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa. Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.
Maoni
Ingia utoe maoni