Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 9 ya Mwaka (Jumatano, Juni 07, 2023)  

Somo la 1

Tob 3:1-10, 16-17

Tobiti alisikitika akalia, na katika huzuni yake aliomba akasema: Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki, na matendo yako yote na njia zako zote ni rehema na kweli, nawe unahukumu kwa kweli na kwa haki milele. Unikumbuke, unitazame; usiniadhibu kwa ajili ya dhambi zangu na makosa yangu; wala kwa ajili ya dhambi za baba zangu walioasi mbele zako. Kwa maana hawakuzitii amri zako; kwa hiyo umetutoa tuwe mateka, hata na kuuawa; kuwa mithali ya shutumu kwao mataifa yote, ambao kwamba tumetawanyika katikati yao. Na sasa hukumu zako zi nyingi na za kweli; hata uje unitende kwa kadiri ya dhambi zangu na za baba zangu; kwa kuwa hatukuzishika amri zako; wala kuenenda kwa kweli mbele zako. Basi sasa unitende kama uonavyo vema; uniamuru niondolewe roho yangu, ili niruhusiwe na kuwa udongo tena; maana yanifaa kufa kuliko kuishi, kwa sababu nimesikia mashutumu yasiyo haki, nami naona huzuni nyingi. Uamuru, basi, nitolewe katika msiba huu, niende mahali pa milele; wala usiugeuzie mbali nami uso wako. Ikawa siku ile ile huko ekbatana, mji wa Media, Sara binti Ragueli naye alishutumiwa na wajakazi wa baba yake. Maana alikuwa ameolewa na waume saba, bali Asmodeo, yule jini, aliwaua kabla hawajalala naye. Wakamwambia, Wewe hujui ya kuwa umewanyonga waume zako? Umekuwa na waume saba, wala hata mmoja wao hukupata faida naye. Mbona waturudia sisi? Ikiwa wao wamekufa, nenda zako nawe ukawafuate; tusikuone kabisa una mwana wala binti. Alipoyasikia hayo alifanya huzuni nyingi, akaona afadhali kujinyonga. Akafikiri, Mimi ni binti pekee wa baba yangu; basi nikitenda hivi nitamwita shutumu; nitamshushia uzee wake kwa huzuni hata kaburini. Basi ikawa sala zao wote wawili zilisikiwa mbele za enzi yake Mungu Aliye juu. Rafaeli akatumwa ili awaponye wote wawili.

Wimbo wa Katikati

Zab 25:2 – 9

Ee Mungu wangu,
Nimekutumaini Wewe, nisiaibike,
Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda.
Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja;
Wataaibika watendao uhaini bila sababu.
(K) Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu.

Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha.
Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu,
Nakungoja Wewe mchana kutwa.
(K) Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu.

Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako,
Maana zimekuwako tokea zamani.
Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu,
Wala maasi yangu.
Unikumbuke kwa kadiri ya ujana wangu,
Wala maasi yangu.
Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako,
Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako.
(K) Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu.

Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake.
(K) Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu.

Shangilio

Mt 11:25

Aleluya, aleluya.
Nakushukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya.

Injili

Mk 12:18-27

Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, walimwendea Yesu, wakamwuliza na kusema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao. Basi kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akatwaa mke, akafa, asiache mzao. Wa pili naye akamtwaa akafa, wala yeye hakuacha mzao. Na wa tatu kadhalika; hata na wote saba, wasiache mzao. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama atakuwa mke wa yupi katika hao? Maana wote saba walikuwa naye. Yesu akajibu, akawaambia, Je! hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu? Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni. Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahi- mu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana.

Maoni


Ingia utoe maoni