Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Bikira Maria, Mama. wa Kanisa (Jumatatu, Mei 29, 2023)  

Somo la 1

Mwa 3:9-15, 20

Baada ya Adamu kule tunda la ule mti, Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala. Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino. Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai.

Wimbo wa Katikati

Zab 87:1-7

Msingi wake upo Juu ya milima mitakatifu.
Bwana ayapenda malango ya Sayuni Kuliko maskani zote za Yakobo.
Umetajwa kwa mambo matukufu, Ee Mji wa Mungu.
(K) Enyi mataifa yote msifuni Bwana.

Nitataja Rahabu na Babeli Miongoni mwao wanaonijua.
Tazama Filisti, na Tiro, na Kushi; Huyu alizaliwa humo.
Naam, mintarafu Sayuni itasemwa,
Huyu na huyu alizaliwa humo.
Na Yeye Aliye juu Ataufanya imara.
(K) Enyi mataifa yote msifuni Bwana.

Bwana atahesabu, awaandikapo mataifa,
Huyu alizaliwa humo.
Waimbao na wachezao na waseme,
Visima vyangu vyote vimo mwako.
(K) Enyi mataifa yote msifuni Bwana.

Injili

Yn 19:25-34

Penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake. Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani. Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake. Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe. Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye. Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji.

Maoni


Ingia utoe maoni