Ijumaa. 21 Juni. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 7 ya Pasaka (Jumanne, Mei 23, 2023)  

Somo la 1

Mdo 20:17-27

Siku zile, toka Mileto Paulo alituma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa. Walipofika kwake, akawaambia, Ninyi wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote, nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi; ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa, bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba, nikiwashuhudia Wayahudi na Wayunani wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo. Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja. Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari njema ya neema ya Mungu. Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huko na huko, hamtaniona uso tena. Kwa hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya mtu awaye yote. Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu.

Wimbo wa Katikati

Zab 68:9-10, 19-20

Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema;
Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu.
Kabila yako ilifanya kao lake huko;
Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa.
(K) Enyi falme wa dunia, mwimbieni Mungu.

Na ahimidiwe Bwana,
Siku kwa siku hutuchukulia mzigo wetu;
Mungu ndiye wokovu wetu.
Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa;
Na njia za kutoka mautini.
(K) Enyi falme wa dunia, mwimbieni Mungu.

Shangilio

Yn 14:16

Aleluya, aleluya,
Nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele.
Aleluya.

Injili

Yn 17:1-11

Siku ile, Yesu aliinua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe. Kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma. Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye. Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako. Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika. Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako. Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao. Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako.

Maoni


Ingia utoe maoni