Masomo ya Misa
Jumamosi ya 3 ya Pasaka (Jumamosi, Aprili 29, 2023)
Mdo 9:31-42
Kanisa lilipata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongoezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu. Hata Petro alipokuwa akizunguka-zunguka pande zote akawatelemkia na watakatifu waliokaa Lida. Akamwona mtu mmoja huko, jina lake Ainea, mtu huyo amelala kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza. Petro akamwambia. Ainea, Yesu Kriso akuponya; ondoka, ujitandikie. Mara akaondoka. Na watu waliokaa Lida na Sharani wakamwona, wakamgeukia Bwana. Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga maogi, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. Akampa mkono, akamwinua, hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai. Ikajulikana katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana.
Zab 116:12-17
Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha wokovu;
Na kulitangaza jina la Bwana.
(K) Nimrudishie Bwana nini kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote.
Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake.
(K) Nimrudishie Bwana nini kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
Mtumishi wako, mwana na mjakazi wako,
Umenifungua vifungo vyangu.
Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
Na kulitangaza jina la Bwana.
(K) Nimrudishie Bwana nini kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Kol 3:1
Aleluya, aleluya,
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
Aleluya.
Yn 6:60-69
Siku ile, watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia maneno ya Yesu juu ya mkate wa uzima, walisema: Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia? Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung’unukia neno hilo, akawaambia, Je! Neno hili linawakwaza? Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima. Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasiomini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti. Akasema, kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.
Maoni
Killian Justus
Very happy for through daily readings to broaden my knowledge about the word of GodIngia utoe maoni