Jumatano. 17 Aprili. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 5 ya Kwaresima (Jumatatu, Machi 27, 2023)  

Somo la 1

Dan 13:1-9, 15-17, 19-30, 33-62

Palikuwa na mtu mmoja jina lake Yoakimu, akikaa Babeli, naye ameoa mke jina lake Susana binti Helkia, mwanamke mzuri sana na mcha Mungu. Wazee wake nao walikuwa wenye haki, pia wamemfundisha binti yao sawasawa na Torati ya Musa. Basi Yoakimu alikuwa mwungwana tajiri, na karibu na nyumba yake alikuwa na bustani nzuri; hivyo Wayahudi humwendea, maana alikuwa ni mwenye heshima kupita wengineo wote. Mwaka ule ule wakaamriwa wawili miongoni mwa wazee wa watu ili kuamua, watu wa namna ile ambao Bwana aliwanena, ya kama ufisadi ulitoka Babeli kwa wazee waamuzi waliohesabiwa kuwa wanatawala watu. Hao walikuwa wakienda mara nyingi kuzuru kwenye nyumba yake Yoakimu; na wote wenye mashtaka yoyote desturi yao wakawajia huko. Basi watu walipoondoka kwenda zao panapo saa sita, Susana huingia katika bustani ya mumewe ili kutembea. Nao wale wazee humwona kila siku anakwenda kutembea; hata wakawaka tamaa kwa sababu yake. Ndipo walipozipotosha nia zao, wakayageuza upande macho yao wasiweze kutazama mbinguni wala kukumbuka hukumu za haki. Ikawa walipongoja wakati wa kufaa, yeye aliingia bustanini kama ilivyokuwa desturi yake pamoja na wajakazi wawili, naye alitaka kuoga kwa sababu kulikuwa na joto. Wala hapakuwa na mtu yeyote isipokuwa wale wazee wawili, ambao wamejificha wakimvizia. Basi akawaambia wajakazi wake, Nileteeni mafuta na sabuni, mkaifunge milango ya bustani ili nioge . Mara wale wajakazi walipokwishas kutoka, wale wazee wawili waliondoka wakamwendea mbio, wakasema, Tazama, milango ya bustani imefungwa asiweze kutuona mtu yeyote nasi tunakupenda sana; haya! Basi, utukubali na ulale nasi. La! Hutaki tutakushuhudia ya kuwa hapa palikuwapo na kijana pamoja nawe, ndiyo sababu uliwaruhusu wajakazi wako. Basi Susana aliugua akasema, Nimesongwa pande zote, maana nikilitenda hilo ni mauti yangu; nisipolitenda siwezi kuokoka mikononi mwenu. Ni afadhali niangukie katika mikono yenu na kukataa, kuliko kutenda dhambi machoni pa Mungu. Mara Susana akapiga kelele kwa sauti kuu; nao wale wazee wawili wakampigia kelele pia. Kisha mmoja wao akakimbia, akaifungua milango ya bustani. Hivyo watumishi wa nyumbani waliposikia kelele bustanini, wao waliingia kwa kasi kwa mlango wa nyuma ili waone ni nini iliyompata. Lakini wale wazee waliisimulia hadith yao nao watumishi wakaona aibu kabisa, kwa maana Susana hakuchongelewa habari ya namna hiyo wakati wowote. Ikawa kesho yake watu walipokusanyika kwa Yoakimu mumewe, wale wazee wawili wakaja nao, wamejaa kusudi lao ovu juu ya Susana la kumfisha. Wakasema mbele ya watu, "Mwiteni Susana binti Helkia, mkewe Yoakim, aje hapa". Basi akaenda kuitwa; naye akaja pamoja na baba yake na mama yake, na watoto wake, na jamaa zake wote. Naye huyo Susana alikuwa mwanamke mwenye adabu, mzuri wa uso; basi hao watu wabaya waliamuru afunuliwe uso, maana alifunikwa utaji, ili washibe uzuri wake. Kwa hiyo rafiki zake na wote waliomtazama wakasikitika. Ndipo wale wazee wawili waliposimama katikati ya watu, wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. Naye akatoka machozi, akatazama juu mbinguni, kwa maana moyo wake ulimtumaini Mungu. Wale wazee wakasema, Sisi tulipokuwa tukitembea bustanini peke yetu, huyu aliingia pamoja na wajakazi wawili, wakaifunga milango ya bustani, naye mara akawaruhusu wajakazi. Kisha kukatokea kijana, ambaye amejificha humo, akamwendea akalala naye. Walakini sisi tungaliko pembeni mwa bustani, tuliona ubaya huo, tukamwendea mbio. Hata tukiwa tumewaona pamoja, yule kijana hatukuweza kumkamata, maana alikuwa mwenye nguvu kuliko sisi, akifungua milango akaepuka. Bali huyu tulimkamata, tukauliza yule kijana yu nani, asikubali kutuambia. Hayo basi, tunashuhudu. Basi waliohudhuria wakawasadiki, wakiwa wazee wa watu na waamuzi; hivyo wakahukumu auawe. Mara Susana akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Mungu wa milele, Wewe wajua yaliyositirika, wajua mambo yote yasijekuwako, Wewe wajua ya kwamba wananishuhudia uongo, na tazama, imenipasa kufa; walakini sikufanya mambo kama hayo, ambayo watu hawa wameyabuni juu yangu kwa ukorofi. Naye Bwana akaisikia sauti yake. Kwa hiyo, alipochukuliwa huyo kwenda kuuawa, Mungu alimchocheleza roho kijana mmoja, jina lake Danieli; naye akapaza sauti akasema, Mimi simo; mimi sina hatia kwa habari ya damu yake mwanamke huyu. Mara wote wakamgeukia, wakasema, Maneno hayo uyasemayo, maana yake nini? Akasimama katikati, akasema, Enyi bani Israeli, mmekuwa wapumbavu, hata kumhukumu binti Israeli bila kuhoji wala kupata hakika ya kweli? Rudini hukumuni; mradi hao wanamshuhudia uongo. Basi watu wote walirejea kwa haraka, nao wale wazee wakamwambia, Njoo uketi kati yetu, utujulishe habari hiyo, endapo Mungu amekupa wewe heshima yam zee. Hapo Danieli aliwaambia, Watu hawa wawili watengwe, nami nitawahoji. Basi wakiisha kutengwa, akamwita mmoja wao akamwambia, Ewe uliyepata kuwa mzee katika uovu, sasa dhambi zako zimekukalia, ulizozitenda zamani kwa kuhukumu isivyo haki, kumpatiliza asiye na hatia na kumwachilia mwovu; lakini Bwana asema, Asiye na hatia, mwenye haki, usimwue. Haya! Basi, wewe ulimwona kwa macho; useme; Chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya msandarusi. Danieli akasema, Hakika umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana sas hivi malaika wa Mungu amepokea hukumu ya Mungu, akukate vipande viwili. akamtenga huyo tena, akaamuru kumleta yule mwingine, akamwambia, Ewe mzao wa Kanaani, wala si wa Yuda, uzuri umekudanganya, na tamaa imeupotosha moyo wako. Hivyo ndivyo ulivyowafanyia binti za Israeli, na kwa hofu walitembea nawe; bali huyu binti Yuda hakuweza kuustahimili uovu wako. Haya! Basi, nawe useme; Chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya mkwaju. Danieli akamwambia, Hakika wewe nawe umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana malaika wa Mungu yu tayari, anakungoja mwenye upanga, akukate vipande viwili; ili awaangamize nyote wawili. Mara hiyo makusanyiko yote wakapaza sauti kwa nguvu, wakamhimidi Mungu awaokoaye wamtumainio. Wakawaondokea wale wazee wawili, kwa maana Danieli ameuhakikisha ushuhuda wao wa uongo hata vinywani mwao wenyewe. Wakawatenda kwa Torati ya Musa kama vile walivyokusudia kwa ukorofi kumfanyia jirani yao; wakawaua; na mwenye damu isiyo na hatia aliokolewa siku ile.

Wimbo wa Katikati

Zab 23

Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
(K) Nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami.

Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza,
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati aya bonde la uvuli wa mauti
Sitaogopa mabaya; kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.
(K) Nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami.

Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe change kinafurika.
(K) Nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami.

Hakika wema na fadhili zinanifuata,
Siku zote za maisha yangu,
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
(K) Nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami.

Shangilio

Yn 6:64, 69

Maneno yako, Ee Bwana, ni roho, tena ni uzima, Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.

Injili

Yn 8:1-11

Yesu akaenda mpaka mlima wa Mizeituni. Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha. Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.

Maoni


Ingia utoe maoni