Masomo ya Misa
Jumanne ya 28 ya Mwaka (Jumanne, Oktoba 11, 2016)
Gal 5:1-6
Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa. Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno. Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote. Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema. Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani. Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.
Zab 119:41, 43-45, 47-48
Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi,
Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako.
(K) Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi
Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe,
Maana nimezingojea hukumu zako.
(K) Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi
Nami nitaitii sheria yako daima,
Naam, milele na milele.
(K) Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi
Nami nitakwenda panapo nafasi,
Kwa kuwa nimejifunza mausia yako.
(K) Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi
Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako,
Ambayo nimeyapenda.
(K) Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi
Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda,
Nami nitazitafakari amri zako.
(K) Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi
Zab 119:135
Aleluya ,aleluya,
Umwangazie mtumishi wako uso wako,
Na kunifundisha amri zako.
Aleluya.
Lk 11:42-46
Yesu aliwaambia Mafarisayo: Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili. Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo. Mtu mmoja katika wana-sheria akajibu, akamwambia, Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi. Akasema, Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu.
Maoni
Ingia utoe maoni