Masomo ya Misa
Jumatatu ya 5 ya Mwaka (Jumatatu, Februari 06, 2023)
Mwa 1:1–19
Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza. Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja. Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji. Mungu akalifanya anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo. Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili. Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo. Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo. Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu. Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili na majira na siku na miaka; tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo. Mungu akafanya mianga miwili mikubwa, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi na kuutawala mchana na usiku na kutenga nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya nne.
Zab 104:1–2, 5–6, 10, 12, 24, 35
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wewe, Bwana, Mungu wangu, umejifanya mkuu sana.
Umejivika heshima na adhama,
Umejivika nuru kama vazi.
(K) Bwana na ayafurahie matendo yake.
Uliiweka juu ya misingi yake,
Isitikisike milele,
Uliifunika kwa vilindi kama kwa vazi,
Maji yalikuwa yakisimama juu ya milima.
(K) Bwana na ayafurahie matendo yake.
Hupeleka chemchemi katika mabonde;
Zapita kati ya milima,
Kando kando hukaa ndege wa angani,
Kati ya matawi hutoa sauti zao.
(K) Bwana na ayafurahie matendo yake.
Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
Kwa hekima umevifanya vyote pia,
Dunia imejaa mali zako.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
(K) Bwana na ayafurahie matendo yake.
Zab 111:7, 8
Aleluya, aleluya,
Maagizo yako yote, ee Bwana, ni amini, yamethibitika milele na milele.
Aleluya.
Mt 6:53-56
Yesu na wanafunzi wake walipokwisha kuvuka walifika nchi ya Genezareti, wakatia nanga. Nao wakiisha kutoka mashuani, mara watu walimtambua, wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo. Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona.
Maoni
Ingia utoe maoni