Alhamisi. 30 Machi. 2023

Masomo ya Misa

Dominika ya 5 ya Mwaka (Jumapili, Februari 05, 2023)  

Somo la 1

Isa 58:7–10

Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri.

Wimbo wa Katikati

Zab 112:4–9

Nuru huwazukia wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki.
Heri atendaye fadhili na kukopesha;
Atengenezaye mambo yake kwa haki.
(K) Nuru huwazukia wenye adili gizani.

Kwa maana hataondoshwa kamwe;
Mwenye haki atakumbukwa milele.
Hataogopa habari mbaya;
Moyo wake u imara ukimtumaini Bwana.
(K) Nuru huwazukia wenye adili gizani.

Moyo wake umethibitika hataogopa,
Hata awaone watesi wake wameshindwa.
Amekirimu na kuwapa maskini,
Haki yake yakaa milele,
Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu.
(K) Nuru huwazukia wenye adili gizani.

Somo la 2

1Kor 2:1–5

Ndugu zangu, mimi nilipopkuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima. Maana naliazimu nisijue neno lolote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa. Nami nalikuwako kwenu katika hali ya udhaifu na hofu na matetemeko mengi. Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili Imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.

Shangilio

Mdo 16:14

Aleluya, aleluya,
Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo.
Aleluya.

Injili

Mt 5:13–16

Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu yam lima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

Maoni


Ingia utoe maoni