Masomo ya Misa
Ijumaa ya 4 ya Mwaka (Ijumaa, Februari 03, 2023)
Ebr 13:1-8
Upendano wa ndugu na udumu. Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua. Wakumbukeni hao waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao; na hao wanaodhulumiwa, kwa vile ninyi nanyi mlivyo katika mwili. Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.
Zab 27:1, 3, 5, 8-9
Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu
Jeshi lijapojipanga kupigana nami,
Moyo wangu hautaogopa.
Vita vijaponitokea,
Hata hapo nitatumaini.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu
Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya,
Atanisitiri katika sitara ya hema yake,
Na kuniinua juu ya mwamba.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu
Bwana, uso wako nitautafuta.
Usinifiche uso wako,
Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira.
Umekuwa msaada wangu, usinitupe,
Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu
Zab 130:5
Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja Bwana, na neno lake nimelitumainia.
Aleluya.
Mk 6:14-29
Mfalme Herode akasikia habari; kwa maana jina lake lilikuwa kutangaa, akasema, Yohana Mbatizaji amefufuka katika wafu, na kwa hiyo nguvu hizi zinatenda kazi ndani yake. Wengine walisema, Ni Eliya. Wengine walisema, Huyu ni nabii, au ni kama mmoja wa manabii. Lakini Herode aliposikia, alisema, Yohana, niliyemkata kichwa, amefufuka. Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa; kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate. Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lo lote utakalo, nitakupa. Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye. Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
Maoni
Ingia utoe maoni