Jumamosi. 27 Aprili. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 4 ya Mwaka (Jumapili, Januari 29, 2023)  

Somo la 1

Sef. 2:3, 3:12 – 13

Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana. Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na masikini, nao watalitumainia jina la Bwana. Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya.

Wimbo wa Katikati

Zab. 146:6b – 10

Huishika kweli milele.
Huwafanyia hukumu walioonewa,
Huwapa wenye njaa chakula;
Bwana hufungua waliofungwa.
(K) Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.


Bwana huwafumbua macho waliopofuka;
Bwana huwainua walioinama;
Bwana huwapenda wenye haki;
Bwana huwahifadhi wageni.
(K) Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

Huwategemeza yatima na mjane;
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele,
Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi.
(K) Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

Somo la 2

1Kor. 1:26 – 31

Ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu. Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi; kusudi, kama ilivyoandikwa, Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana.

Shangilio

Yn. 14:5

Aleluya, aleluya,
Tomaso akamwambia Bwana, Sisi hatujui uendako, nasi twaijuaje njia?
Aleluya.

Injili

Mt. 5:1 – 12a

Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, Heri walio maskini war oho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; maana hao watafarijika. Heri wenye upole; maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema; maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni.

Maoni


Ingia utoe maoni