Ijumaa. 26 Aprili. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 3 ya Mwaka (Jumapili, Januari 22, 2023)  

Somo la 1

Isa 9:1–4

Hapo kwanza aliingiza nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa tukufu, karibu na njia ya bahari; ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa. Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangaza. Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, kama furaha ya wakati wa mavuno, kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara. Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midani.

Wimbo wa Katikati

Zab 27:1, 4, 13-14

Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

Neno moja nimelitaka kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana
Siku zote za maisha yangu.
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

Somo la 2

1Kor 1:10–13, 17

Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu husema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizawa kwa jina la Paulo? Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristu usije ukabatilika.

Shangilio

Mt 4:23

Aleluya, aleluya,
Kristo alihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.
Aleluya.

Injili

Mt 4:12–23

Basi Yesu aliposikia ya kwamba Yohane amefungwa, alikwenda zake mpka Galilaya; akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali: ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa, Watu wale waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti mwanga umewazukia. Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye, ambao walikuwamo chomboni pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita. Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata. Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya Ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.

Maoni


Ingia utoe maoni