Alhamisi. 28 Machi. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 2 ya Mwaka (Jumamosi, Januari 21, 2023)  

Somo la 1

Ebr 9:2–3, 11–14

Hema ilitengenezwa, ile ya kwanza, mlimokuwa na kinara cha taa, na meza, na mikate ya Wonyesho; ndipo palipoitwa, Patakatifu. Na nyuma ya pazia la pili, ile hema iitwayo Patakatifu pa patakatifu. Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng’ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?

Wimbo wa Katikati

Zab 47:1–2, 5–8

Enyi watu wote pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe.
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote.
(K) Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, na Bwana kwa sauti ya baragumu.

Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu.
Mwimbieni Mungu, naam, imbeni,
Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni.
(K) Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, na Bwana kwa sauti ya baragumu.

Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote,
Imbeni kwa akili.
Mungu awamiliki mataifa,
Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu.
(K) Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, na Bwana kwa sauti ya baragumu.

Shangilio

Kol 3

Aleluya, aleluya,
Neno la Kristu likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote; mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.
Aleluya.

Injili

Mk 3:20-21

Yesu aliingia nyumbani na mkutano wakakusanyika tena, hao wao wenyewe wasiweze hata kula mkate. Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili.

Maoni


Ingia utoe maoni