Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 1 ya Mwaka (Ijumaa, Januari 13, 2023)  

Somo la 1

Ebr 4:1–5, 11

Ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na Imani ndani yao waliosikia. Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile; kama vile alivyosema, Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, hawataingia rahani mwangu; ijapokuwa zile kazi zilimalizika tangu kuwekwa misingi ya uolimwengu. Kwa maana ameinena siku ya saba mahali Fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na hapo napo, Hawataingia rahani mwangu. Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu yeyote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi.

Wimbo wa Katikati

Zab 78:3–4, 6–8

Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu,
Ambayo baba zetu walituambia,
Tukiwaambia kizazi kindine
Sifa za Bwana na nguvu zake.
(K) Msiyasahau matendo ya Mungu.

Wasimame na kuwaambia wana wao,
Wamwekee Mungu tumaini lao,
Wala wasiyasahau matendo ya Mungu,
Bali wazishike amri zake.
(K) Msiyasahau matendo ya Mungu.

Wasiwe kama baba zao,
Kizazi cha ukaidi na uasi,
Kizazi kisichojitengeneza moyo,
Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu.
(K) Msiyasahau matendo ya Mungu.

Shangilio

Yn 17:17

Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya.

Injili

Mk 2:1-12

Baada ya siku Yesu akaingia tena Kapernaumu. Ikasikiwa ya kwamba Yesu alikuwa nyumbani. Wakusanyika watu wengi, isibaki nafasi hata mlangoni; akawa akisema nao neno lake. Wakaja watu wakimletea mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne. Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza. Naye Yesu, alipoiona Imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Na baadhi yay a waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao, Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu? Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu? Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza), Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende nyumbani kwako. Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Namna hii hatujapata kuiona kamwe.

Maoni


Ingia utoe maoni