Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 3 ya Majilio (Alhamisi, Desemba 15, 2022)  

Somo la 1

Isa 54:1-10

Imba, wewe uliye tasa, wewe usiyezaa; paza sauti yako kwa kuimba, piga kelele, wewe usiyekuwa na utungu; maana watoto wake aliyeachwa ni wengi kuliko watoto wake yeye aliyeolewa, asema Bwana. Panua mahali pa hema yako, na wayatandaze mapazia ya maskani yako; usiwakataze; ongeza urefu wa kamba zako; vikaze vigingi vya hema yako. Kwa maana utaenea upande wa kuume na upande wa kushoto; na wazao wako watawamiliki mataifa; wataifanya miji iliyokuwa ukiwa kukaliwa na watu. Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena. Kwa sababu Muumba wako ni mume wako; Bwana wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote. Maana Bwana amekuita kama mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako. Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya. Kwa ghadhabu ifurikayo nalikuficha uso wangu dakika moja; lakini kwa fadhili za milele nitakurehemu, asema Bwana, Mkombozi wako. Kwa maana jambo hili limekuwa kama maji ya Nuhu kwangu; maana kama nilivyoapa ya kwamba maji ya Nuhu hayatapita juu ya dunia tena, kadhalika nimeapa ya kwamba sitakuonea hasira, wala kukukemea. Maana milima itaondoka, na vilima vitaondolewa; bali wema wangu hautaondoka kwako, wala agano langu la amani halitaondolewa; asema Bwana akurehemuye.

Wimbo wa Katikati

Zab 30:1, 3-5, 10-12

Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua,
Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
Umeniinua nafsi yangu, Ee Bwana, kutoka kuzimu.
Umenihuisha na kunitoa Miongoni mwao washukao shimoni.
(K) Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua.

Mwimbieni Bwana zaburi, Enyi watauwa wake.
Na kufanya shukrani. Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.
Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,
Katika radhi yake mna uhai. Huenda kilio huja kukaa usiku,
Lakini asubuhi huwa furaha.
(K) Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua.

Ee Bwana, usikie, unirehemu, Bwana, uwe msaidizi wangu.
Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;
Ee Bwana, Mungu wangu, Nitakushukuru milele.
(K) Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua.

Shangilio

Lk. 3:4, 6

Aleluya, aleluya,
Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake, na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu.
Aleluya.

Injili

Lk 7:24-30

Wajumbe wa Yohane walipokwisha ondoka, Yesu alianza kuwaambia makutano habari za Yohane, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Jueni, watu wenye mavazi ya utukufu, wanaokula raha, wamo katika majumba ya kifalme. Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia, na aliye zaidi ya nabii. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako. Nami nawaambia, Katika wale waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohane; lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye. Na watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohane. Lakini, Mafarisayo na wana-sheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye.

Maoni


Ingia utoe maoni