Masomo ya Misa
Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili (Alhamisi, Desemba 08, 2022)
Mwa 3:9-15, 20
Baada ya Adamu kule tunda la ule mti, Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala. Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino. Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai.
Zab 98:1-4
Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe, Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake, Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
(K) Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote, Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K) Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Efe 1:3-6, 11-12
Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu.
Lk 1:28
Aleluya, aleluya,
Salamu, Mariamu, ulipewa neema. Bwana yu pamoja nawe! Umebarikiwa katika wanawake.
Aleluya.
Lk 1:26-38
Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
Maoni
Ingia utoe maoni