Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 2 ya Majilio (Jumanne, Desemba 06, 2022)  

Somo la 1

Isa 40:1–11

Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu, asema Mungu wenu. Semeni na moyo wa Yerusalemu, kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa, kwa kuwa amepokea kwa mkono wa Bwana adhabu maradufu kwa dhambi zake zote. Sikiliza ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni nyikani njia ya Bwana, nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu. Kila bonde litainuliwa, na kila mlima na kilima kitashushwa; palipopotoka patakuwa pamenyoka, na palipoparuza patasawazishwa. Na utukufu wa Bwana utafunuliwa, na wote wenye mwili watauona pamoja, kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya. Sikiliza, ni sauti ya mtu asemaye, Lia! Nikasema, Nilie nini? Wote wenye mwili ni majani, na wema wake wote ni kama ua la kondeni. Majani yakauka, ua lanyauka, kwa sababu pumzi ya Bwana yapita juu yake. Yakini watu hawa ni majani. Majani yakauka, ua lanyauka, bali neno la Mungu wetu litasimama milele. Wewe uuhubiriye Sayuni habari njema, panda juu ya mlima mrefu; wewe uuhubiriye Yerusalemu habari njema, paza sauti kwa nguvu. Paza sauti yako, usiogope; iambie miji ya Yuda, Tazameni, Mungu wenu! Tazameni, thawabu yake I pamoja naye, na ijara yake I mbele zake. Atalilisha kundi lake kama mchungaji, atawakusanya wanakondoo mikononi mwake; na kuwachukua kifuani mwake, nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.

Wimbo wa Katikati

Zab 96:1–3, 10–13

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana likarikini jina lake,
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
(K) Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa.

Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake.
Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki,
Atawahukumu watu kwa adili.
(K) Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa.

Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo.
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha.
(K) Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa.

Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi,
Atahukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake.
(K) Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Siku ya Bwana i karibu, Tazama atakuja kutuokoa.
Aleluya.

Injili

Mt 18:12–14

Siku ile, Yesu aliwaambia wafuasi wake. Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi wale tisa na tisini, akaenda milimani, na kumtafuta yule aliyepotea? Hata akipata kumwona, amin, nawaambia, amfurahi huyo zaidi, kuliko wale tisa na tisini wasiopotea. Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.

Maoni


Ingia utoe maoni