Masomo ya Misa
Jumatatu ya 2 ya Majilio (Jumatatu, Desemba 05, 2022)
Isa. 35:1-10
Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa Bwana, ukuu wa Mungu wetu. Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na mchanga ung’aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji; katika makao ya mbweha, walipokuwa wamelala, patakuwa na majani, pamoja na mianzi na manyasi. Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo. Hapo hapatakuwa na simba, wala mnyama mkali hatapanda juu yake; hawataonekana hapo; bali waliokombolewa watakwenda katika njia hiyo. Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitamkimbia.
Zab. 85:8-13
Nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawaambia watu wake Amani.
Naam, na watauwa wake pia,
Bali wasiurudie upumbavu tena.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.
(K) Tazama Mungu wetu atakuja na atatuokoa.
Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na Amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni.
(K) Tazama Mungu wetu atakuja na atatuokoa.
Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.
(K) Tazama Mungu wetu atakuja na atatuokoa.
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Tazama Mfalme, Bwana wa ulimwengu, Yeye ataiondoa nira ya utumwa wetu.
Aleluya.
Lk. 5:17-26
Ikawa siku zile, Yesu alikuwa akifundisha, na Mafarisayo na waalimu wa torati walikuwa wameketi hapo, waliotoka katika kila kijiji cha Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu; na uweza wa Bwana ulikuwapo apate kuponya. Na tazama, wakaja watu wanamchukua kitandani mtu wmenye kupooza; wakataka kumpeleka ndani na kumweka mbele yake. Hata walipokosa nafasi ya kumpeleka ndani kwa ajili ya lile kundi la watu, walipanda juu ya dari wakampitisha katika matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda chake katikati mbele ya Yesu. Naye alipoiona Imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako. Basi, wale waandishi na Mafarisayo wakaanza kuhojiana wakisema, Ni nani huyu asemaye maneno ya kukufuru? N’nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake? Na Yesu alijua hoja zao, akajibu akawaambia, Mnahojiana nini mioyoni mwenu? Lililo jepesi ni lipi? Kusema, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwmbia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako. Mara hiyo akasimama mbele yao, akajitwika kile alichokilalia, akaenda zake nyumbani mwake, huku akimtukuza Mungu. Ushaangao ukawashika wote, wakamtukuza Mungu; wakajaa hofu, wakisema, Leo tumeona mambo ya ajabu.
Maoni
Ingia utoe maoni