Masomo ya Misa
Jumanne ya 1 ya Majilio (Jumanne, Novemba 29, 2022)
Isa 11:1-10
Siku ile litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawanya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia. Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kimono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe. Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira. Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari. Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzika patakuwa na utukufu.
Zab 72:1-2, 7-8, 12-13, 17
Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
Na mwana wa mfalme haki yako
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu.
(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi na wingi wa amani kwa milele.
Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka mto hata miisho ya dunia.
(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi na wingi wa amani kwa milele.
Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi,
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
Na nafsi za wahitaji ataziokoa.
(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi na wingi wa amani kwa milele.
Jina lake na lidumu milele,
Pindi ling’aapo jua jina lake liwe na wazao;
Mataifa yote na wajibariki katika yeye,
Na kumwita heri.
(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi na wingi wa amani kwa milele.
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Tazama Bwana wetu atakuja na nguvu, na atayaangaza macho ya watumishi wake.
Aleluya.
Lk 10:21-24
Siku ile, Yesu alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia. Akawageukia wanafunzi wake, akasema nao kwa faragha, Heri macho yaonayo mnayoyaona ninyi. Kwa kuwa nawaambia ya kwamba manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi wasiyasikie.
Maoni
Ingia utoe maoni